USINITESE BURE.

Kwa Muhibu. 

Natumai u salama. Mimi sijambo. Baba na mama wote wazima. Hawana neno. Juzi mama kanitani, “Ah, Collian mwanangu, ni lini utaleta lazizi tumkague?” Asema eti kila mara mimi huandamana na rafiki wa kiume tu. Nikamweleza kuwa ni asuburi tu, kwani hivi karibuni atamkaribisha mwenzangu nyumbani, yaani wewe.

 Natamani sana kukuona angalau nitulie. Mwenzangu,  umeumbwa ukaumbika. Ngozi nyororo, ngozi ya rangi ya maji ya kunde, kimo chako sawia. Macho yako yapendeza. Yametameta kwa mahaba. Tabasamu lako lavutia si kidogo. Laweza mchanganya na kumchangamsha mwanamume yeyote duniani.

Licha ya hayo mpenzi, ninayo hoi, nina  masikitiko makubwa na sononeko la moyo. Naugua ila sina maradhi. Buheri wa afya mwenzako. Sononeko langu ni kwa ajili yako. Ulinichezea  sere kwani? Wakumbuka siku nilipokusuhubia? Nawe ukakiri kuwa utakuwa mpenzi wangu? Ukaniahidi kuwa tutashirikiana katika kukuza uhusiano wetu ili baadaye tuijenge familia? Umekwenda kimya. Tena kimya chako kimekidhiri. Kimezidi. Kando na hayo, hauitikii simu. Jumbe kwenye WhatsApp haujibu. Kitu gani kinachoendelea mpenzi?


Madhumuni ya kuandika  barua hii ni kukuuliza maswali  yafuatayo. Ulighairi nia au ungali kipenzi changu cha roho? Je, ulipata mwema kuniliko na ukakosa kunambia? Wanifikiria niliko au mimi ndiye ninayejisumbua bure?

Sitaki kuishi katika fantasia mbali katika uhalisia wa mapenzi.Sitaki siku moja uje kuniatua moyo, nipandwe na jitimai, nibaki ukiwa na mengi ya kusema. Nikose kujifaa kwa lolote wala chochote kama aliyefiwa.

Nieleze  ukweli uniweke huru. Unifungue mwili na mawazo. Dhana za kupendwa nawe zinitoke akilini. Japo utaniumiza mtima kwa kunisaliti, nitapoa baada ya muda. Tusidanganyane. Tafadhali nieleze kama bado tupo pamoja?

Siwezi kamwe kujisukumia kwako. Hilo fahamu. Nikajaribu utanipa penzi la kinafiki. Nalo penzi la aina hio lina vitushi vyake. Tena ni sumu. Nieleze kama hunipendi niugue mtima nipone mapema. Sitaki tudanganyane au tutiane vidonda nyoyoni vitakavyo tutonesha kila uchao. Kijana mdogo mahali nilipo naogopa maisha ya misukosuko.

Nieleze  ukweli sasa. Ukweli wa moyo, sio wa mdomoni. Je, ungali unanipenda au ulinitupa kwenye kaburi la sahau? Kama ndio wanipenda, nionyeshe kwa vitendo. Kama ni udhaifu fulani nitarekebisha na kama ni maumbile unichukue nilivyo au uniteme. Nende kwa amani, nawe katafute kwingine. Maana kudanganywa kuna machungu yake. Na katika machungu hayo kipo kinyongo kinachochanganyika na hasira. Kumbuka  hasira ni bomu. Ikilipuka lazima matangazo yatapeperushwa hewani. Kwenye mitandao, redio na kwenye runinga kuwa; Mpenziye kamtoa uhai.

Kama sijui kupenda basi nieleze watu husoma mapenzi kwenye chuo gani. Pengine kama kipo Chuo Kikuu cha Mapenzi. ( Nadharia na Ufundi.) Tafadhali nipevushe. Nielekeze ili nijisajilishe nipate shahada za uzamili na uzamifu. Nieleze ni vipi unataka kupendwa. Fungua roho. Tangaze msimamo manake siwezi kwenda mbele wala kurudi nyuma pasipo kusikia msimamo wako.

Hatimaye, kama ukaniacha kwa dosari zangu, ni sawa. Sina ubaya lakini kumbuka pia nawe una kasoro za kwako. Sikulaani wala usinielewe vibaya. Mtu asiyetosheka daima huyumbishwa na mawimbi yaitwayo tamaa. Nayo tamaa ni maradhi hatari kuliko kaswende na kisonono. Huangaisha mtu hadi kaburini.

Wako “mpendwa”

Collian Andrew Muli.

muliandrew01@gmail.com

Makala haya yamehaririwa na

Vinky Mshairi.

Karumimwaniki@students.Ku.ac.ke

Asante kwa kusoma hadi tamati. 

Tuzidi kusemezana.

Advertisements

10 thoughts on “USINITESE BURE.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s